Kenya Baada ya Miaka 48

Yapata miaka arbaini na minane tangu nchi yetu ipate uhuru, jambo ambalo tungefaa kujivunia. Hata hivyo ni huzuni kubwa kuyaona tunayoyakabili; uchochole, ufisadi, ubadhirifu wa mali ya umma na mengineyo. Dhidi ya dhana ya Mkenya aliyeishi miaka tulipojinyakulia uhuru, imekuwa ni mambo ya kushangaza yanayovuta maendeleo yetu nyuma. Mataifa mengine ya Kiafrika huenda yakawa aidha yametushinda kwa maendeleo ama ustawi.

Ni huruma iliyo kubwa kwa Mkenya anayeongozwa na mafisadi. Manufaa gani kujikomboa kutoka mikononi mwa mabeberu na hatimaye kujifunga pingu za ufisadi? Hili ni jambo la fedheha. Juzi tu tuliposikia kiwango kikubwa cha fedha kimetoweka kutoka wizara ya elimu. Ukitafakari haya huenda ukatasikia mengine kutoka idara tofauti. Hili ni jambo ambalo nilidhani tulikwishajinasua punde tu baada ya utawala wa wakoloni. Hili ni jambo ambalo limesheheni asilimia kubwa ya idara za serikali na kibinafsi hapa nchini. Mwananchi wa kawaida kama mimi hawezi kukidhiwa haja bila chai al-maarufu Kitu-Kidogo. Ndiyo maana wasio na ‘nafasi’ wanazidi kuwa wakata wasio na matarajio ya kuiona kurunzi ya neema maishani mwao.

Hili jambo linawiana na lile la ukabila. Kwa sasa ni kama Kenya imekuwa ya makabila fulani huku mengine yakiwa kama si muhimu. Kulingana na mimi, Wakenya wote ni sawa. Uwe Mkamba, Mluhya ama Mjaluo. Jambo la ukabila halifai kutenganisha kwa makundi wananchi.

Tutazame wabunge tulio nao kwa mfano. Tunazidi kuelekea kwenye dimbwi la giza na maafa kwa kuwachagua viongozi wasiofaa. Yupo mbunge wa Gatundu Kaskazini asiyejua vema kusoma wala kusema lugha rasmi zinazotumika bungeni. Hii ni kama kumchagua bubu bungeni ama kutarajia kuongozwa na kipofu. Kama lugha za mawasiliano hazielewi, ikawaje alichaguliwa na kuingia bungeni?

Mwenzake wa Makadara ni mwengine ambaye amezua vioja kwa jina la kuwatetea vijana wenzake. Kama kiongozi anayefaa kuhishimiwa hastahili kuwa na tabia zinazofanywa na wenzake mitaani. Wengine wa wabunge pia wakihusishwa na mambo tofauti tofauti yaliyo kinyume cha maadili yanayotakiwa katika jamii; kutajwa kama walanguzi wa dawa za kulevya, kuhusishwa na vifo vya Wakenya wasio na hatia, kuhusika katika ufisadi ukabila na mengineyo.

Wabunge hawa ndio wanaokwepa kulipa kodi. Hili linamwudhi mwananchi wa kawaida anayetozwa kiwango kikubwa cha mapato yake madogomadogo. Pesa hizi zinapoingia kwenye hazina ya serikali, ndizo zinatumia kwa ubadhirifu na mwishowe kutoweka kama ilivyofanyika katika wizara ya elimu.

Hali ngumu ya maisha pia imezagaa kote nchini na kushinikiza janga la umaskini. Shilingi ya Kenya imekosa thamani na bei za vyakula na bidhaa zote kwa jumla kuwa juu; huduma za kawi, karo, nauli nk. Hili linasababisha wengine kujitoa uhai na kuziacha familia zao zikiteseka na kuangamia. Wengine hufa njaa bila angalau tone la maji wala tonge la ugali. Badala ya baadhi ya viongozi wetu kuwajibika na suala la ufadhili kwa waadhiriwa, utawapata kwenye juhudi za malumbano na siasa zisizowanufaisha Wakenya hao.

Imewahi kutokea kuwa bidhaa zinazotolewa kama misaada kwa waadhiriwa wa ukame na njaa hazifiki. Nyinginezo huuziwa njiani kwa manufaa ya watu binafsi, wenzao wanapopambana na hali ngumu ya maisha inayowakabili. Hii ni kujitakia laana kubwa inayonata miaka nenda miaka rudi kwa familia na vizazi vyao vijavyo.

Pengo lililopo kati ya matajiri na maskini linazidi kuongezeka bila matajiri kuwa na huruma kwa maskini wala kuwajali. Hujitia hamnazo wawapatapo na kukuwanyanyasa wanaowahudumia. Matajiri hawa ndio hugombea viti vya ubunge kwa kuwanyenyekea ama kuwahonga wapiga kura wasio na uwezo wa kifedha. Waingiapo bunge huwasahau waliowachagua mashinani na kuwarejelea tena uchaguzi unaofuata.

Kenya inazidiwa na unyonge wa kila aina. Tafakari suala la Migingo na Ugingo. Pasipokuwa na viongozi watakaopigania haki, viziwa hivi na vinginevyo vitazidi kunyakuliwa na nchi jirani kupitia kwa viongozi wao wanaodhaniwa kuwa marafiki wetu.

Juzi tu katiba mpya iliidhinishwa lakini kufuatiliwa na kutekelezwa limekuma jukumu lisilo la maana Kwao. Hawa ni viongozi wanaoongoza kwa midomo tu lakini vitendo vyao kamwe haviambatani.

Ilidhamiriwa kwa umero na uongozi wa udikteta ulikuwa umefika mwisho lakini sivyo. Iwapo hujui, wangalipo ‘wakoloni weusi’ wanaowagandamiza wananchi. ‘Wakoloni’ wenyewe walijitapia na kujinyakulia mashamba makubwamakubwa na mali ya umma kwa jumla. Kwa sasa wengine wangali maskwota kwenye mashamba yayo hayo na wengine hawana hata vijishamba wanavyoviita vyao ili wajenge ama wavitumie hata kuchimbiwa makaburi yao.

Tutazidi kumwomba Mwenyezi Mungu ili atuepushie maovu bali atuneemeshe. Nina matumaini, inshaallah,  ya kuona Kenya iliyo na mabadiliko. Tafakari hayo.

Ongeza Maoni Yako