Victor Mulama; Bingwa Anayeghani Mashairi

Victor Mulama ni mshairi ambaye amesikika akighani mashairi katika idhaa ya Radio Maisha kwenye kipindi cha Nuru ya Lugha  na  baadhi ya mashairi kuchezwa kwenye  kipindi cha Ramani ya Kiswahili K.B.C Redio taifa. Mashairi yake yametumika kwenye tamasha za mziki. Pia  amealikwa kwenye baadhi ya makongamano na warsha za Kiswahili, harusi, sherehe mbalimbali na hata katika shule mbalimbali nchini ili kuwahamasisha wanafunzi. Ameandaa DIMBWI LA USHAIRI-kanda  ya mashairi ambayo yaonekana kuwa diwani ya kwanza ya sauti nchini. Victor hufanya kazi na Standard Media Group baada ya kuhitimu katika chuo kikuu cha Mount Kenya University bewa la Eldoret alikosomea utangazaji.

Victor Mulama almaarufu Malenga wa Mabondeni, alizaliwa mwaka wa 1991, Juni 26. Ni mvulana wa pekee katika familia ya wana watatu. Lakabu yake ya kuwa malenga wa mabondeni yatokana na sababu kuwa alizaliwa na kulelewa katika bonde la ufa mjini Nandi Hills. Hii ni kufuatia kuajiriwa kwa wazazi wake katika kiwanda cha majani chai Chemomi Tea Estates. Pia Mulama anaamini kwamba utunzi wake ulianzia kiwango cha chini anakoita mabondeni’ambapo hakupata mlezi wa  mapema kumlea vizuri katika ushairi. Kitovu  cha uzawa wa malenga huyu ni Kakamega,magharibi ya taifa la Kenya.

Victor alifanya mtihani wake wa KCPE katika shule ya msingi Masiyenze katika eneo bunge la Ikolomani. Baadaye akajiunga na shule ya kirafiki Friends High School Shiveye-Kaklamega ambapo alimalizia pale na kupata gredi ilomwezesha kujiunga na chuo kikuu cha Mount Kenya mwaka wa 2013 ili kusomea kozi ya utangazaji na mawasiliano.Amekuwa ripota wa nyanjani akiwa idhaa ya BHB Radio 96.3 fm ilokuwa mjini Eldoret mwaka wa 2014 hadi pale ilipohamishwa kujiunga na BHB Radio 96.7 fm Nairobi mwezi wa Novemba. Victor Mulama alikuwa mwalimu katika shule ya kibinafsi Assurence Academy Eldoret mwaka wa 2012 na 2013 akifundisha somo la Kiswahili na Dini [CRE] katika madarasa ya juu.

Haikuwa rahisi kwa Victor Mulama kujiunga chuoni.Baada ya Victor kuhitimisha masomo ya sekondari, aliajiriwa kuwa kitwana katika boma la mtu wakati huo akichanga pesa za kwenda kusomea udereva.  Baadaye akachukuliwa na mjomba wake ili kwenda kumchungia kuku wa kutaga mayai katika boma lake. Hapo Mulama akaanza kubadili ndoto na kutaka kuwa mwalimu maishani.Hata hivyo,aliishia kusomea kozi ya utangazaji na mawasiliano baada ya kushauriwa na walimu waliomfunza. Misingi ya kushauriwa ilitokana kwa walimu kumwona akiwa mbunifu na msemaji mzuri haswa baada ya kuhutubia kwa ujasiri shuleni katika hafla ya kuwaaga walimu.

Malenga huyu alishiriki tamasha za mziki akiwa shuleni na kwenye sherehe za Krisimasi,jambo lililompa mduduizo wa kupenda mashairi. Alianza safari yake ya utunzi akiwa darasa la saba mwaka 2006 katika shule ya msingi Masiyenze chini ya ulezi wa mwalimu wake Destereous Isindu almarufu Isindu wa Isindu-Mzee Mufti. Pia Matthias Momanyi alikuwa mshauri wake wa karibu kuanzia mwaka wa 2012 wakati aligundua Victor kuwa na uwezo wa kutunga mashairi kupitia kitandazi . Aidha Hassan Mwana wa Ali ameshiriki pakubwa katika kumkuza malenga huyu  kwa kucheza mashairi yake kwenye kipindi cha Nuru ya Lugha. Kwa mashairi mengi aliyoyatunga,yanayokumbukwa ni Majambazi wa Injili,Yebei Tokeza, Mbunge Wangu, Mwili usinisumbue,Watu wa Pembe na Sijataka Kujipamba.

Victor amewasilisha mashairi kwenye makongamano, tamasha, warsha, harusi na pia kualikwa katika shule mbalimbali ili kusema na wanafunzi. Ushairi umemfanya kuzuru maeneo mengi nchini ili kuburudisha na kuelimisha wengi. Ughani wake alijifunza kwa kuiga sauti za washairi kama mzee Abdalla Mwasimba na Nuhu Bakari ndipo baadaye akapata mtindo wa pekee wa kucheza na sauti yake anapoghani. Anashikilia kwamba ni kosa kuwasuta wanaojifunza jambo kwa kupinga hamu zao bila kuwapa njia mbadala ya kujikuza.

“Washauri wakandamizaji huua hamu za wadogo kuiga wakubwa wao eti wawe wabunifu.Mimi siamini kwamba kuna kosa katika kuiga mtu anayeathiri talanta yako kwa uzuri. Mtu huiga akitaka kuwa bora kama fulani na katika hali ile akabuni mtindo wake wa kipekee mwishowe. Hujui kuogelea bila kuig waliobobea kuogelea.Waliofaulu wote waliiga ndipo wakafika waliko. Hivyo ni kosa kupinga na wengine kufuata maguu ya ya vielelezo vyao maishani.Iga na ubuni yako. Sanaa si milki ya mtu”.

Ushauri  wa Victor Mulama kwa washairi chipukizi na vijana kwa ujumla ni kutia bidii katika masomo huku wakikuza talanta zao mbalimbali. Anapendekeza washairi kutilia maanani malumbano ya kuangazia mada zinazofaa kuelimisha jamii wala si vita vya kudhalilishana mtandaoni.

”Tofauti baina ya watunzi wa jadi na wa leo ni kuwa zamani washairi walipendana na kulumbana kwa kupimana welewa wa maswala yanayoathiri umma. Watunzi wa leo wanalenga watu. Dhima ya ushairi si kutusiana bali ni kuelimisha,kuburudisha na kufaa jamii kwa jumla”.

Victor anaaamini kuwa Kiswahili si chombo cha mawasiliano tu bali pia chombo cha burudani. Kwa kuwa ushairi huelimisha, Victor ametoa kanda ya mashairi ya kimsamiati ili kufanya wepesi wa kuelewa  majina mbalimbali ya Kiswahili mfano msamiati wa ukoo, malipo na sayari.

Victor ni mraibu wa kusoma, kutizama runinga na kuimba mashairi. Victor ni mwana Chealsea na  Fc Leopards. Ili kuwasiliana na Victor Mulama tumia nambari 0702244042.

Zifuatazo ni baadhi ya beti za mashairi yake.

Nataka kitu Fulani,adhimu kwa moyo wangu,
Narambita kwa imani,anirehemishe Mungu,
Naomba niwe fanani,anijaze wema wangu,
Nataka niwe barua,nisomwe mbele na nyuma.

Nisomwe mbele na nyuma,kwa wadogo na wakubwa,
Nionwe mwenye Huruma,nisiwe kama majibwa,
Nipigane na umoma,nilete vilivyoibwa,
Nataka niwe barua,nisomwe mbele na nyuma

Nia ni kubadilika,mwaka mpya mambo mapya,
Nanga imeshakazika,nang’oa kwenda kwa upya,
Neno ni kutakasika,nifanywe kiumbe kipya,
Nataka niwe barua,nisomwe mbele na nyuma.

Ongeza Maoni Yako