Jamii ya Kizazi Kipya

Najihurumia kuwa katika jamii iliyojaa misukosuko ya kisiasa, ukabila na majanga tofauti. Hili ni jambo ambalo limeniumiza moyo sana na kunipa mshawashawa kuandika makala haya. Haifani unapoishi katika jamii iliyojaa waasi, wahuni na waroho. Huenda ikawa ni shinikizo watu wa maeneo haya wanyoyapata kutoka kwa viongozi wao.

Uvivu ni mojawapo ya mambo yanayoathiri taswira ya maeneo haya. Naam! Haikosi pia ukosefu wa bidii kama si uvivu. Hili ndilo linalochangia na kushinikiza maovu yanayotendwa na watu. Vijana barobaro walio na siha kutosha ila hafai mtu yeyote sembuse wao wenyewe. Hawana kazi za kufanya kutwa na hawajishughulishi kwa lolote kupata kazi wala riziki. Hao ndio hupata muda wa kupiga gumzo mchana kutwa kuhusu wanasoka, wanasiasa ama hata kupanga njama za wizi. Mara wakae kitako wakizungumzia maswala yasiyowafaidi ama wataniane ili kupisha muda. Hiyo ndio jamii ya kisasa.

Vijana hawa huwaabudu wanasoka kiwango cha kutafuta mabango ya picha zao na kuyatundika kwenye viambaza vya vyumba vyao. Wengine huchongeza sanamu kana kwamba ndio miungu. Hawapati hata lepe la usingizi wakitazama kandanda kwenye vilabu usiku kucha. Kama wangalikuwa kazini mchana hawangalipata muda usiku wa kuzuru maeneo hao wakati wa usiku. Namaanisha wangeona ni vema wapumzishe nafsi zao wakati wa giza. Kwenye hivyo vyumba vya vileo hutawakosa majambazi sugu wakijadiliana na kunoa makali ama wakishindana mwenye ujuzi zaidi. Wanawake nao na mavazi yasiyoonesha maadili wana lengo lao huko. Aidha wakitafuta riziki ama wakisambaza magonjwa yasiyo na tiba. Wengine husimama karibu na nguzo za majumba mijini wakiwasubiri wateja wao. Hao ni wateja wanaotoka kazini, wachovu na wenye bidii za mchwa kwa kazi zao. Bila huruma, wanawake hao huwapora hela walizokuwa wakitafuta kwa jasho jingi. Si neno.

Vijana wasipojadili ya wanasoka, watajadili ya wanasiasa. Mijadala hii pia ni kwa wazee waliopata muda wa udaku. Wanaume wakongwe huelezea waliyoshuhudia wakati wa wakoloni wakilinganisha na serikali za kisasa zilizojaa wahuni, waroho na viongozi wengine wenye tamaa ya kiwango cha juu. Wanasiasa huabudiwa mno kiwango cha kutumainiwa kwa yatayojiri. Hao viongozi ndio husinikiza vita vya kikabila au vya kidini. Ifikapo hapo ndio wajuao sana hii lugha hushopoa mambo kama haya; mwenye nguvu mpishe.

Wanasiasa wengine huonyesha utengano kwa wazalendo ila wenyewe ni masahibu wanaothaminiana mno. Mzalendo naye na uzalendo wake anazidi kuumia akiihurumia nchi yake. Huyu ndiye mzalendo hubadilika na kuwa mwasi anayeidharau nchi yake. Waja wa Mungu ni wengi.

Wanawake nao hawaachwi nyuma kwa juhudi zao za udaku wakieneza chuki. Kwenye biashara zao za kuuza vitumbua au makaa hupiga gumzo na wateja wao kwa hali ya juu. Mtu humjui na za kwako wamwelezea. Huo ndio wakati wataelezana kuhusu wanaume na mambo mengine wanayoyaenzi. Wachache wanaotambua ya siasa wataonesha ujuzi wao usiomfadi yeyote.

Ukitaka kumficha Mwafrika chochote, kifiche kwa maandishi aliyesema kauli hii alijua. Licha ya juhudi za serikali kujenga maktaba za umma, vitabu katu havisomwi vikamfaidi mtu. Ni wakutubi tu na rafu zao! Wanafunzi ndio haooo. Vilabuni na cyber wakitazama filamu za ngono. Ati walimu nao? Wanabugia pombe haramu zinazipofusha, kuua na kupunguza nguvu za kiume. Sitaki pia kutaja ukarimu wa wanafunzi wa kike wa walimu wa kiume. Lakini nitaje tu wanavyopatiwa alama za bure kwenye mitihani kwa masharti ya raha zao. Iwapo unadhani napiga chuku, huenda uliathirika kwa moja ama nyingine.

Mtoto uleavyo ndivyo akuavyo. Mdekeze. Akiitisha kuku mchinjie. Akitaka vibanzi mpatie. Kutwa moja utajuta. Nilikozaliwa sikuswifu mno lakini wazazi wangu walijua msemo mmoja tu; mtoto akililia wembe mpe. Hizo zilikuwa siku za ‘usimwekee mtoto kiboko chini ‘. Kwa mamangu haikuwa kiboko tu, ila chochote kilochomfaa kumlainisha mwanawe. Sisemi kamba tu ya kufungia kuni bali hata mwiko wa jikoni. Nami kwa ni ‘mguu niponye’. Nikifikiwa, ni mimi tu n Mungu wangu.

Ni nyakati ambazo taadhima imefifia. Mtume mtoto atakujibu atakavyo. Nyakati za kitambo zilipita. Kwenye mabasi watoto waliwapa wakubwa viti. Heri wasimame. Siku hizi hata mtoto ana kiti chake mle ndani. Na kama hana, atakukalia kwenye mapaja kana kwamba ni haki yake. Ndio hao watoto wanaokuamuru waonavyo wazazi wao wakifanya. Lakini kila mvulana ni baba wa kesho msichana mama wa kesho. Ndio maana hufanya watakavyo.

Vijana ndio wamepita mipaka. Mara ninaposafiria matatu hutafuta isiyo na muziki. Na kama ni muziki, ni sauti ya chini. Vijana hutafuta magari yenye muziki kwa sauti ya juu na iwapo utatoa maoni, utaarifiwa kuwa umezeeka. Kama utaelewa wasemavyo, utakuwa umebahatika. Lugha zao si lugha. Labda ni kwa sababu hawataki ‘wazee’ waelewe wanachokisema ama wachangie kwa mazungumzo yao yasiyo na maadili.

Baadhi ya nyimbo wanazozitukuza ni za ajabu. Waimbaji nao wana dunia yao. Mitindo yao mipya imewaelekeza vijana kwenye dimbwi la anasa zinazowabadilisha mawazo na kufikiri kama wazungu. Baadhi ya wanamuziki hao huabudu shetani hivyo basi huwarai washabiki wao kumwabudu huyo kiongozi wao. Ishara zao za mikono na picha kwenye mavazi yao zinadhihirisha hayo. Mimi namjua kiongozi mmoja tu! Aliyeziumba mbingu na nchi. Huenda ikawa vijana wetu watabadilishwa bila ya idhini yao wenyewe. Hii ndio hatari inayowakabili hawa viongozi wa kesho. Nawaita viongozi wa kesho kwa sababu kila mtu huwa na lengo na ndoto ya maisha yake. Lakini kati ya hizo ndoto, ni gani hutimia? Lakini hata sisi tulipokuwa wachanga ilikuwa hivyo tu. Kila mtu aliwaza na kuwazua jinsi angependa kuwa katika maisha ya baadae. Wengine walipenda sana kuwa walimu wakini walijipata mitaani wakiuza njugu. Aliyekuwa na ndoto ya kuwa rubani sasa hivi ndiye huyo mchuuzi. Hakuna aliyekuwa na doto ya kuwa duni maishani lakini hilo limewafuata. Na masomo waliosoma? Sielezi kuwa hayawafaidi, lakini ni wachache wamenfaika nayo.

Usijifanye malaika kwamba hujawaona wasichana wa vyuo na mitindo yao ya mavazi. Mapaja wakiyaonyesha labda kwa wanaume watakaowapa pesa ili wawahudumie. Maziwa nje utadhani fundi wa nguo hakuijua sana kazi yake. Na kama hiyo nguo ndefu, yaonyesha kilicho ndani na kilichodhamiriwa kusetiriwa. Basi kuna haja gani ya kuivaa. Nadhani hili limetokana sana Wazungu. Wasichana wa Kiafrika nao wakataka kuwa Wazungu kwa mavazi, mawazo na mitindo mbalimbali. Suruali ndefu zinazowabana ni kama hizi zilishonewa miilini mwao. Kila mkunjo wa ngozi unajionesha wazi. Kama ni viatu ni vile vyenye visigino vya twiga. Akitembea sauti inamfuata. Ka! Ka! Ka! Hili pia ninamkwaza kwa kuwa hawezi kukimbia. Sketi fupi nazo utadhani zinampa uhuru wa kutembea atakavyo?

SIku moja nilipoabiri basi, dada akaketi kando yangu. Ile minisketi yake ikawa fupi kupindukia. Nilimwona akijaribu kuyaficha mapacha yake na viganja vya mikono. Kucha nazo ndefu na zenye rangi asiweze kushika mapeni ya kulipa nauli. Nampongeza dreva mmoja aliyemshurutisha kondakta wake asimwabirishe dada aliyekuwa na mavazi ya aina hiyo. Nadhani huyo ni mmojawapo wa madreva wachache walioko kwenye ukanda huu.

Nywele za wanawake ndizo wanazothamini sana. Ukitaka vita toa maoni dhidi ya hizo nywele. Wanawake watafanya juu chini kupata pesa ili wazinunue. Zinakotoka hizo nywele hujui. Hujui wanatumia nini kuziunda. Lakini kinachostaajabisha zaidi ni muda zitakaa kwenye vichwa vyao ukikumbuka haiziwezi zikaoshwa kwa maji. Huo nao si chafu? Kumbe wanaojikwatua na kujipamba wanaonekana kuwa warembo lakini uchafu umejaa kichwani. Naam! Ndio maana utawapata na marashi yanayonukia ili kuzuia mnuko wa uchafu vichwani.

Wanawake wengine ama hao hao hujipaka waja na rangi tofauti tofauti kila mahali kwa miili yao. Wengine wanapofunga macho utaona rangi zilizokolea juu ya macho kama huyu hakuoga vizuri. Kucha ndizo hizo na rangi tofauti. Na hizo kucha nyingine huenda ni za kubandika. Wengine huchorwa na kuchomwa picha za wanyama mbalimbali aidha kwenye vifua, mikono au miguu. Hujui hao wanyama wana ishara gani. Labda ni baadhi ya wanyama wanaotumiwa na watu wanaoabudu shetani. Ishara hizo huwa hazitoki ng’o – mpaka kifo kiwatenganishe na ulimwengu. Wanawake hawa hupita mipaka kwa marashi. Sisemi tu wanawake! Wanaume ni wengine. Kuna wakati utatapika uwapi ndani ya matatu paingiapo kiumbe kama huyo wa kuhurumiwa.

Wanaume hawaachwi nyuma kwa nywele. Wamezisuka utadhani ni wanaume. Nyingine zimepakwa rangi usijue huyu kijana ni mti au kiumbe wa aina gani. Vijana hawa pia hujipamba kwa mapambo mengine usijue kama ni wanaume ama ni wanawake isipokwa uwaangalie tu kwa makini vifua vyao. Haya ndiyo mambo mkengeuko. Yanayofanywa na wanawake ni wanaume. Yanayofanywa na wanaume ni ya wanawake. Mungu atuhurumie.

Dunia kweli imebadilika. Simu za rukono zimeharibu mambo yote. Utawapata hawa vijana wakizitumia kupasha ujumbe usio na busara. Mara wakizitumia kuingia kwenye mitandao ya kijamii. Mitandao hii ya kijamii wanaitumia isivyopaswa. Wengine hutekeleza majukumu yao ili wapate muda zaidi ya kuingia kwenye mitandao hiyo. Huko ndiko utapata makala tofauti na chuki ikiwasilishwa kutoka kwa jamii hii hadi nyingine. Wengine wanapotumia hizi simu hutumia uongo. Mara niko hapa, mara niko pale. Kwa sababu mnayewasiliana naye hakuoni. Hizi ndizo simu pia hutumiwa kuwatapeli wasiotambua mambo kwa haraka. Ole wao!

Vijana hao hao huenda kwenye vyumba vya burudani yakiwepo naeneo ya kuonyeshwa filamu. Si filamu za kuwajenga kiroho bali ni za kuwapotosha. Hizo ndizo zinaelekeza kwenye jaa la mazito yasiyo na suluhu. Vijana hawa hujaribu kuiga matukio ya filamu hizi wasijue yana utata. Wanavyojionea watukipigana risasi kunawaunda majambazi wa kesho na si viongozi wa kesho. Iwapo hao ndio wazazi wa kesho, basi vizazi vyetu havitaidumisha heshima, upole na maadili. Msione tu nalalamika ila jaribuni tu kutafakari ninayowaeleza.

Walio na umaskini hufanya juhudi zao kujiondoa kwenye masaibu hayo. Wengine huwatembelea waganga watajika. Waganga nao wakishindania ujuzi wa kubandika vibao na matangazo yao mitaani. Kumbe si jambo na ujuzi ama utendakazi. Ni nipe nikupe. Wakati huu ikiwa nipe hela nikupe huduma. Mganga anaposhindwa kwa huduma zake humwitisha mteja wake kitu atakachosa ili asirudi tena. Kuku wa kijani hupatikana wapi? Labda umpake rangi!

Niruhusu tu nikudokezee ya uzazi. Mama mjamzito amevaa suruali ndefu inayombana. Nguo maalum za wazazi hawa zimetelekezwa. Cha kushangaza zaidi ni huyu mwanamke kuvuta sigara, kutumia vileo na dawa za kulevya. Hiki kitoto hakina haki! Mbona umnyime haki mtoto kwa mambo ya muhimu hata kabla hajazaliwa?

Mtoto anapozaliwa ni mengine. Kwanza mamake atapendelea kitendo cha upasuaji kuliko kitendo cha kawaida cha kumkopoa huyu mwana. Akizaliwa huanza maisha yake mapya kwenye hii dunia iliyojaa kero na karaha. Majirani, majamaa na marafiki huitwa kupiga vigelele kumshangilia huyu mwana aliyeteswa kutoka tumboni. Kwa bahati njema, atapata lishe njema ambayo hupatikana tu kwa tukizi. Atavalishwa nguo zilizotumiwa na wenzake waliomtangulia ama zilizonunuliwa sokoni. Hizi ndizo nguo zinazotolewa ng’ambo, ambazo Wazungu wamezitumia.

Nakumbuka siku moja nikiwa abiria wa pikipiki almaarufu bondabonda. Baada ya mkasa mdogo wa ajali, tuliendelea na safari yetu. Tulikopitia kulikuwa porini. Miti tu na wanyama hapa na pale. Tulikutana na baba na mwanawe wa miaka mitano hivi wakielekea tulikotoka. Dereva wa pikipiki akasita kidogo na kuwatazama. Walivyotembea ilidhihirisha wazi walikuwa wachovu. Dereva akanieleza aliwaona wakienda. Akaniarifu walikuwa wakirudi. Hili jambo liliniatua moyo sana. Iweje mtoto wa miaka mitano anatembeza kilomita tano kwenda na kilomita tano kurudi. Mawazo hayakunihurumia. Iwapo huyo mtoto alikuwa amepelekwa hospitalini? Babake hangepata shilingi mia mbili za kumlipa mhudumu wa pikipiki? Iwapo alishindwa kugharamia nauli,  mtoto huyo alikuwa amenunuliwa chakula? Haya ndiyo masaibu katika jamii hii.

Wazazi watamlea mwana kwa kumdekeza ama kwa kumnyanyasa. Huyu ndiye mtoto atasoma kama karo itapatikana kishaye alipiwe hongo ili apate kazi. Ufisadi imekuwa kama haki. Kila mtu na hoja yake. Asiye na dinari si mwananchi. Kama pesa ziko atakuwa mwananchi na iwapo ana nafasi kubwa kwa pesa na mali, basi ni mwenye nchi.

Tazama matatu zinapopita. Askari huko barabarani na haki zake. Asipoipata hizo haki zake, dereva, kondakta na abiria wote wamo mashakani. Imefika pale tunasema ‘toa kitu kidogo nikuoneshe njia’. Usidhani ni barabarani tu! Hospitalini kuna wauguzi na madaktari. Usipokuwa na hicho kitu kidogo huhudumiwi. Iwapo huyu mgonjwa humo taabani, kafani ndipo pake na mwishowe kaburini. Mtoto unapomwingiza shuleni utatozwa ada hiyo hiyo. Unapojiunga na kikosi cha polisi mambo ni hayo hayo. Maofisa wa afya hukuidhinisha kwa njia hiyo hiyo. Wanasiasa kuingia kwenye nyadhifa zao ni hivyo hivyo. Ifikapo hapo, mnyonge hukosa nafasi na kubaki kwenye dimbwi la umaskini. Namaanisha maskini jungu la mavi na mkorogowe.

Ukibahatika kupata kazi, mateso yameanzia. Usidhani mshahara utakufaa kwa vyovyote. Kiwango cha huo mshahara ni kidogo sana. Umfanyie kazi mwajiri wako, umtajirishe, akudharau. Maoneo wanayofanyia hizo kazi ndio ya kushangaza. Kwa mfano, walioajiriwa kwenye mashamba ya maua hutumia kemikali. Iwapo hizi kemikali zitakuathiri sifa yako ififie, hapo ni wewe tu na Mungu wako. Mwajiri lake tu ni kutaka kujua kama maua yanaendelea kukua, kupaliliwa, kunyunyiziwa dawa na kuchanua. Wewe na ugonjwa wako utaelekezwa kwenye zahanati humo humo shambani kisha urejeshwe shambani kuendeleza kazi yako. Naam! Hakuna atakayeomba ruhusu aseme haji kazi ati anaenda hospitalini kwa maana zahanati i papo hapo.

Nyanyangu aliyeaga dunia miaka ishirini na sita iliyopita hakuyaacha haya. Kawa anaweza kufufuka huenda akafa tena asitamani kufufuka mara ya pili. Haya ndio mambo yanayoendelea kwenye jamii ya kisasa. Jamii wa kizazi kipya!

Ongeza Maoni Yako