Ujana Haudumu

Leo tarehe 06/03/2017 ilikuwa siku ya buriani kwa Gavana wa kwanza jimbo la Nyeri, Nderitu Gachagua. Licha ya shughuli nyingi, niliamua kuwa na wakati ili kufuata yaliyojiri wakati wa tukio hilo la kumuaga Gavana.

Yalikuwa mazishi ya kwanza kwa mtu wa cheo hicho hapa nchini Kenya chini ya katiba mpya iliyozinduliwa mwaka wa 2010. Wengi walitaka kujua yatakayojili kwa tukio la aina hiyo. Baada ya kifo chake naibu wake Balozi Wamaathai alikuwa ameshaapishwa kuwa Gavana wa pili wa Nyeri.

Matukio yalikuwa si haba, nao muda ukawa mwepesi wa kwenda upesi. Magavana thelathini na watano na viongozi wengine wengi wakahudhuria ili kushuhudia kuagwa kwa mwenzao. Wengi walitoa hutuba zao kwa umati uliojaa ukumbi hadi pomoni.

Japo wengi walitoa rambirambi kwa hutuba zao, raisi mstaafu Mwai Kibaki hakutaja jambo kama hilo. Alionekana kukosa siha na maneno yake kutoeleweka na watu kwa hotuba yake ya dakika kumi hivi.

Yamkini alikuwa na maana ya undani kwa hotuba yake ijapokuwa wengi walitoa maoni ya kutoridhika na hotuba hiyo.

“Tuko kwa mambo ya maana sana…” Huyo aliyejulikana kwa ucheshi alianza hotuba yake ambayo wengi kwa mitandao ya kijamii walitoa maneno ya kejeli.

Hotuba yake ilirejelea ukweli na uongo wa wanasiasa wanaoahidi wapiga kura. Ni vema kuyasikiliza maneno ya mzee na kuyatafakari. Usimcheke mzee kwa kuwa ujana ukienda haurudi. Jambo hili lilinikumbusha shairi hili la Shaaban Robert.

Ujana kitu kitamu, tena ni azizi sana,
Maungoni mwangu humu, nilikuwa nao jana,
Kwa wingi katika damu, tahamaki leo sina,
Nasikitika hadumu, rafiki yangu ujana

Kichwa kimejaa mvi,kinywani meno hamna,
Nikenda kama mlevi, miguu nguvu haina,
Kumbe ujana ni hivi, ukenda hauji tena,
Nasikitika hadumu, rafiki yangu ujana

Jua langu limekuchwa, na nyota nilizoona,
Ukinitazama kichwa, nywele nyeusi hakina,
Kama zilizofikichwa, zikang’olewa mashina,
Nasikitika hadumu, rafiki yangu ujana

Natatizika kauli,midomo najitafuna,
Nimekusanya adili, walakini hali sina,
Dunia kitu bahili, hiki una kile huna,
Nasikitika hadumu, rafiki yangu ujana

Nilikuwa ni waridi, furaha ya wasichana,
Neno hawakunirudi, wakati wa kukutana,
Sasa nanuka baridi, wanionapo waguna,
Nasikitika hadumu, rafiki yangu ujana

Walio wakinihusu, walikuwa wengi sana,
Wanawake wenye busu,uzuri na usichana,
Leo sina hata nusu, ya wanitajao jina,
Nasikitika hadumu, rafiki yangu ujana

Wazuri wenye uturi, na mikono yenye hina,
Kila mtu mashuhuri, alipenda kuniona,
Nilifaa kwa shauri, na sasa kauli sina,
Nasikitika hadumu, rafiki yangu ujana

Dunia bibi harusi,kwa watu kila namna,
Inapendeza nafsi, wakati wa kuiona,
Na leo sina nafasi, kwa uzee kunibana,
Nasikitika hadumu, rafiki yangu ujana

Kilichokuwa gizani, niliweza kukiona,
Nikakijua thamani, sura yake hata jina,
Leo sijui ni nini, hata ikiwa mchana,
Nasikitika hadumu, rafiki yangu ujana

Kilichotaka fikra, niliweza kukinena,
Kwa mfano na kwa sura, mpaka kikafanana,
Leo tazama hasara, nguvu hiyo sina tena,
Nasikitika hadumu, rafiki yangu ujana

Kilichotaka mapimo, sikifahamu mapana,
Marefu yake na kimo, siifahamu bayana,
Nusu nimo nusu simo, duniani najiona,
Nasikitika hadumu, rafiki yangu ujana

Hadumu nasikitika, rafiki yangu ujana,
Machozi yamiminika, na kutenda hapana,
Ni wakati umefika, uzee dawa hauna,
Nasikitika hadumu, rafiki yangu ujana

Hauna dawa uzee, mabega yamepetana,
Anionaye ni ‘wee”, ondoka hapa laana,
Wanaposema na miye, niliyekuwa na jina!
Nasikitika hadumu, rafiki yangu ujana

Kaditamati shairi,uchungu wanitafuna,
Walakini nafikiri, twafuata Subuhana,
Katika ile amri, ya “kuwa” na “kutengana”
Nasikitika hadumu, rafiki yangu ujana

(Shaaban Robert, Tanga)

Ongeza Maoni Yako