Anayeumia ni Mpiga Kura

Tunapopiga kura si kwamba tu tunafanya zoezi la kidemokrasia bali ni kuchagua viongozi wema watakaotuwakilisha vilivyo. Isiwe ni jambo la mazoea kuamka mapema siku hiyo ili uwapiku wengine kwenye safu ndefu za Wakenya wengine wazalendo.

Licha ya wanasiasa kuwarai wapiga kura kutekeleza wajibu wao inapaswa pia ifahamike wazi umuhimu wa kupiga kura. Wengi wetu wamefanya zoezi hilo kwa muda mrefu sana bila kuona matunda yake. Wengine tukijuta na wengine kulalamika kwa matendo ya udhalimu ya viongozi tunaowachagua.

Sijawa kwenye zoezi hili kwa miaka mingi lakini mara kadha ambayo nimepiga kura ni dhibitisho kuwa nafahamu machache ninayoandika kwenye makala haya. Viongozi tunaowachagua, wakati mwingine wametupuuza na kutusahau punde tu wanapoapishwa. Hivi ni kumaanisha kuwa viongozi hao wanawania kujinufaisha tu na kuyajaza matumbo yao bila kuwashughulikia wananchi waliowachagua.

Wakati mwingine huwa ni vigumu kuchagua utakayempigia kura ila suala la ukabila ndilo jambo kuu linalotumiwa katika uamuzi huo. Si kwamba wachagua kura ni wakabila ila viongozi ndio huainisha wapiga kura kulingana na lugha zao za mama.

Viongozi hawa wawili anapoingia uongozini hujinufaisha wenyewe bila kushughulikia nafsi za waliowachagua. Mpiga kura naye huselea kwenye umaskini bila mtu anayewajali. Mali ya huwa huharibiwa bila kujali.

Sijaona wamefaa, wabunge mnochaguwa,
Barazani watakaa, wanene kutambuliwa,
Watazamie kung’aa, ya umma kung’ang’aniwa,
Hata mkalia njaa, za umma yaharibiwa!

Mifukoni zinajaa, vema wakihudumiwa,
Wanaodhaniwa taa, mwanga umefunikiwa,
Kazi wameikataa, wakikosa cha kuliwa,
Hata mkalia njaa, za umma zaharibiwa!

Njaa nayo yasambaa, wazalendo wanafiwa,
Kwingine wanapumbaa, wakata wamezidiwa,
Wafa bila kukomaa, pasi na kusaidiwa,
Hata mkalia njaa, za umma zaharibiwa!

Za kondoo wamevaa, waja hamjagunduwa,
Maovu wanaandaa, vita haramu kuzuwa,
Waulize kuhadaa, viongozi watajuwa,
Hata mkalia njaa, za umma zaharibiwa!

Wengine watanyamaa, hawataki jisumbuwa,
Wametuletea baa, hatari bila kujuwa,
Hawanalo la ridhaa, hawa tumewatambuwa,
Hata mkalia njaa, za umma zaharibiwa!

Tunabaki kuzubaa, shida ni kujielewa,
Kwa wingi wana tamaa, watakazo hupatiwa,
Hutaka cha manufaa, kwa mengi wakisifiwa,
Hata mkalia njaa, za umma zaharibiwa!

© Kimani wa Mbogo, 2011

Mtetezi wa mpiga kura ni nani? Kiongozi mwema na atakayefanya kulingana na matakwa ya mwananchi ndiye nani?

La muhimu ni kumpigia kura kiongozi anayejulikana kwa kuwa na rekodi njema ya huduma kwa mwananchi. Si kwa sababu ni mmoja kutoka kwa kabila lako.

Ongeza Maoni Yako