Umaarufu wa Shaaban Robert

Kila linapotajwa jina lake, dhana ya ubingwa inayohusu lugha ya Kiswahili hutanda mawazoni. Shaaban Robert alichangia kwa mengi ambayo hata sasa yangali yanakumbukwa na wengine kuenzi maisha yake. Shaaban anakumbukwa kama bingwa aliyechangia katika lugha ya Kiswahili kwa kazi zake za fasihi, ambazo kufikia sasa, asilimia kubwa imekusanywa na kuchapishwa kwenye vitabu mbalimbali. Baadhi ya vitabu hivyo vimetumika na wanafunzi wa shule na vyuo nchini Tanzania na nchi nyinginezo ambako Kiswahili hufunzwa.

Wasifu wa Shaaban Robert

Shaaban Robert alizaliwa 1909 katika kijiji cha Vibambani kata ya Machui, kilomita kumi kusini mwa Tanga, nchini Tanzania. Inaaminika wazazi wake walikuwa wa asili ya kabila la Wahiyao na ukoo wa Mganga kutoka mikoa ya Tanzania kusini iliyobobea sana katika desturi na mila za Uswahili.

Hata hivyo, jina la babake Robert, ambalo ni la Kikristo halieleweki wazi asili yake kwa kuwa ukoo wao ulikuwa wa Waswahili na Waislamu halisi. Kunao wanaoamini kuwa alipata jina hilo shuleni ila wengine hutoa maoni tofauti.

Wapo baadhi wanaosimulia kuwa asili ya jina Robert ni mwajiri wa babu yake ambaye aliitwa ‘Roberto’ aliyekuwa na Mwitaliano. Nyanya yake Shaaban alipokuwa mjamzito alipatikana sana ufukweni. Huko ndiko alikojifungua kwa msaada wa wanakijiji. Kwa sababu hiyo, baba yake Shaaban alipatiwa jina la Ufukwe. Lakini alipokwenda kazini kumpa taarifa hiyo mwajiri wake, mzungu huyo alitaka sana mtoto huyo aitwe jina lake “Roberto”.

Jina la Ufukwe likafifia. Alipomzaa Shaaban, akawa akipenda sana kumwita Shaaban Roberto. Alipoingia shuleni, ambazo zilienzi sana Kingereza, ikawa Shaaban Roberts, majina ambayo aliyatumia kwa kipindi kifupi. Katika ukubwa wake, akaanza kutumia majina yake kama Shaaban Robert, anavyojulikana mpaka leo.

Shaaban Robert alipata elimu yake katika shule ya Msimbazi jijini Dar es Salaam kati ya mwaka 1922 na 1926 alikofanya vizuri sana na kupata cheti cha kuhitimu. Mwaka wa 1926 aliajiriwa kama karani katika Idara ya Forodha ya Serikali ya Waingereza. Alifanya kazi katika bandari tofauti zikiwemo Pangani na Bagamoyo.

Kati ya 1944 na 1946 alihamia Mjini Morogoro katika ofisi za mbuga za wanyama. Kati ya 1946 na 1952 alifanya kazi mjini Tanga katika idara ya mipango  kabla ya kustaafu utumishi wa umma.

Kwa umahiri wake wa uandishi, chama cha TANU kilimtumia kuhamasisha kwa kutumia kipaji chake cha ushairi. Ni jambo linaloaminika kumvutia sana Mwalimu Nyerere.

Shaaban Robert alikuwa na wake watatu katika vipindi tofauti, Amina, Sharifa binti Hussein na Mwanambazi binti Alii. Amina (1930-1931) alitokea ukoo wa mwalimu Kihere, walizaa watoto wengi lakini waliobahatika kuishi ni wawili, yaani Mwanjaa na Suleimani. Amina Alifariki 1942. Sharifa binti Husein aliyemuoa 1945 alitokea Chumbageni Tanga. Walizaa naye watoto wanne; Akili, Hussein, Mwema na Ikibari. Mke huyu alifariki 1955. Mwanambazi binti Alii naye alitokea Tongoni Tanga, hakuzaa na ndiye aliyemkalia eda Shaaban na alifariki baadaye mwaka wa 1964.

Shaaban Robert alifariki Juni 22, 1962 akiwa na umri wa miaka 53, kwa maradhi ya moyo na upungufu wa damu. Alizikwa katika kijiji cha Machui, Vibambani.

Tuzo alizozipata Shaaban Robert
 1. Margaret Wrong Memorial Prize for Writing.
 2. Tuzo ya Member of the British Empire (MBE) – hii ni heshima na kupata uraia ya nchi ya Uingereza.
 3. Tuzo ya Fasihi kutoka kwa Mwalimu Nyerere kwa mchango wa jamii ya Tanganyika (Tanzania baadaye), lakini tayari alikuwa ameshafariki.
“Hakuwa mtumwa wa lugha za kigeni”

Shaaban Robert alitumia lugha asili ya Kiswahili bila kuegemea lugha nyinginezo za kigeni. Watumiaji wengi wa Kiswahili leo hii, wamekuwa wakichanganya Kiswahili na lugha za kigeni, hasa Kiingereza. Wengi hudai kuwa lugha ya Kiswahili ina uhaba wa maneno, hivyo basi kuegemea suala la kutumia maneno ya kigeni. Hili ni jambo ambalo Shaaban Robert hakulifanya katika uandishi wake.

“Shaaban Robert hakufanya hivyo, yeye alijikita katika lugha yake ya Kiswahili licha ya kuzifahamu baadhi ya lugha za kigeni; na bado amebaki kuwa mtu maarufu mwenye heshima kubwa huku akienziwa. Pale alipotumia lugha ya kigeni katika uandishi wake, alikuwa na sababu za msingi, hasa kuonyesha mtindo katika kazi zake.” anaelezea msomi mmoja katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.

Kazi zake za Fasihi

Katika uhai wake, Shaaban aliandika tungo nyingi za Hadithi Fupi na Mashairi. Zinazopatikana ni jumla ya vitabu 24.

Kazi yake ya kwanza aliitoa mwaka 1932 katika gazeti la mamboleo. Ilikua barua kwa mhariri. Kazi hii aliipa jina la Hirizi ya Shilingi Mia. Ilihusu kupinga ushirikina. Kazi hii inapatikana katika kitabu cha Barua za Shaaban Robert.

Katika tungo zake nyingi,  Shaaban Robert alilenga sana utu, nafasi ya mwanamke katika jamii, ukombozi wa bara la Afrika, kukuza lugha ya Kiswahili na maendeleo. Taasisi ya Uchunguzi wa Kiswahili (TUKI) ya chuo kikuu cha Dar es Salaam imekuwa ikikusanya kazi zake kwa lengo la kuchapishwa.

Dada yake Mwana Saumu anaelezea hivi: “Mimi mwenyewe, (Shaaban) aliniusia kazi ya kukusanya kazi zake, nami nimekusanya zote nilizoweza kupata. Katika kuzipanga nimepata mashaka mengi, ndipo ikanibidi nieleze kama hivi kanuni nilizofuata. Ni wazi kwamba Shaaban alipangakazi zake kwa uangalifu sana nami sikubadili kamwe mpange wake isipokuwa, kwa mfano, kama shairi moja likitokea katika vitabu viwili au zaidi, ndipo nikatia humu kila kipande mara moja tu nikifuata maneno yake kama yalivyokwisha sahihishwa; hivi ni kwamba desturi yake alisahihisha maandishi yake mara nyingi.” Kielezo cha Fasili Uk x.

Ifuatayo ni orodha ya vitabu vya Shaaban Robert:

 1. Almasi za Afrika (1971), Nelson, Nairobi
 2. Koja la lugha(1969), Nelson, Nairobi
 3. Insha na mashairi,(1967), Nelson, Nairobi
 4. Kielezo cha Fasili, (1962), Nelson, Nairobi
 5. Pambo la Lugha, (1968), Oxford, Nairobi
 6. Ashiki Kitabu Hiki, (1968), Nelson, Nairobi
 7. Mashairi ya Shaban Robert, (1971), Nelson, Nairobi
 8. Sanaa ya Ushairi, (1972), Nelson, Nairobi
 9. Mwafrika Aimba, (1969), Nelson, Nairobi
 10. Masomo Yenye Adili, (1959), Art & Literature, Nairobi
 11. Mapenzi Bora, (1969), Nelson, Nairobi
 12. Tenzi za Marudi Mema na Omar Khayyam(1973), TPH, Dar es Salaam
 13. Utenzi wa Vita vya Uhuru(1961), Oxford, Nairobi
 14. Almasi za Afrika na Tafsiri ya Kingereza (1960), Art & Literature, Nairobi
 15. Maisha yangu na baada ya miaka hamsini, (1949), Nelson, Nairobi 
 16. Adili na Nduguze,(1977) TPH, Dar es Salaam 
 17. Kusadikika (1951),Nelson, Nairobi 
 18. Kufikirika (1968) Nelson, Nairobi  
 19. Wasifu wa Siti bint Saad (1967) Art & Literature, Nairobi 
 20. Utu bora mkulima,(1968) Nelson, Nairobi 
 21. Siku ya watenzi wote (1968) Nelson, Nairobi 
 22. Barua za Shabani Robert 1931-1958 (2002), TUKI, Dar es Salaam 
 23. Kielezo cha Insha (1954) Witwatersrandd, Nairobi 
 24. Methali na mifano ya Kiswahili, (2007), TUKI, Dar es Salaam
Sifa za Jina lake
 1. Rais wa kwanza wa Tanzania Mwalimu Julius Kambarage Nyerere alidhamini kazi zake na kuziingiza kwenye kumbukumbu za historia nchini Tanzania.
 2. Barabara inayoelekea Ikulu pia inajulikana kama “Barabara ya Shaaban Robert.”
 3. Shule ya upili ya Shaaban Robert inapatikana jijini Dar es Salaam katika barabara ya Magore. Ni shule iliyoanzishwa tarehe 14/05/1963.
 4. Kuna mitaa ya Jiji la Dar es Salaam na mikoa mingine inayojulikana kwa jina la Shaaban Robert kwa lengo la kumuenzi.

Licha ya Shaaban Robert kujulikana;

 1. Kaburi lake halina hadhi ya jina lake. Kwenye kaburi hilo, hakuna ishara yoyote inayoonyesha kuwa aliyezikwa hapo ni mtu maarufu.
 2. Baadhi ya watu wa familia yake waliwahi kusimulia kuwa hakuna manufaa yoyote yanayopatikana kwa familia ya Shaaban Robert hata kutoka kwa nchi mbalimbali duniani wanaokwenda kuzuru kaburi lake.
 3. Licha ya umuhimu wa Shaaban kwa taifa la Tanzania, hakuna juhudi zinazofanyika ili kuendelea kumuenzi.

Ongeza Maoni Yako