Lahaja za Kiswahili

Lahaja ni namna ya lugha ambayo inasemwa katika eneo moja la nchi ambapo ni tofauti katika maneno au sarufi, kinyume na aina nyingine ya lugha hiyo. Kulingana na Kamusi Sanifu ya Isimu na Lugha (1990:21), Lahaja ni kitarafa cha lugha kinachobainika kijamii au kijiografia na kudhihirishwa na vipengele maalumu vya kisauti na kimuundo.

Lahaja za lugha moja hutofautiana katika matamshi, miundo ya sarufi na msamiati. Lahaja ni kitarafa cha lugha kinachobainika, kijamii au kijiografia na hudhihirishwa na vipengele maalumu vya sauti. Iwapo lugha hutofautiana katika matamshi tu, tofauti hizo huitwa lafudhi, si lahaja. Uchambuzi na uchanganuzi wa lahaja ni tawi la isimujamii.

Hizi ni baadhi ya sababu ambazo husababisha kuzuka kwa lahaja:
 • Kijiografia – Wazungumzaji wa lugha huweza kutawanyika katika maeneo tofauti kwa matakwa yao binafsi au kwa kutenganishwa na maumbile ya kijiografia kama kisiwa, mito au mipaka ya kisiasa. Tofauti hii husababisha kuzuka kwa lahaja na pengine masikilizano yakiwa hafifu baada ya muda fulani lugha huzuka.
 • Uwezo wa Kiuchumi – Hili ni kufuatia matabaka ya kijamii, ngazi ya elimu na kazi, umri, mazingira ya nyumbani na malezi. Watu wa kipato cha chini au wenye elimu duni hutumia zaidi lugha isiyo rasmi. Wenye elimu na kipato hutumia zaidi lugha rasmi katika mawasiliano.
 • Tofauti za Rangi na Jinsia – Ubaguzi baina ya tabaka au jinsia moja na nyingine hupelekea kuwepo kwa vizuizi baina ya matabaka hayo na hivyo kuzua tofauti za kilahaja. Kwa mfano, nchini Marekani watu weusi wana lahaja yao tofauti inayotambulika.
Zifuatazo ni baadhi ya lahaja za Kiswahili:
 1. Kimiini (Mwiini, Barawa) – Kusini mwa somalia
 2. Kitikuu (Bajuni, Gunya) – Mpakani mwa Kenya na Somalia
 3. Kisiu – Kisiwa cha pate
 4. Kipate – Kisiwa cha pate kusini-magharibi
 5. Kiamu – Kisiwa Lamu (kaskazini)
 6. Kishela  – Kisiwa cha Lamu
 7. Kimatondoni  – Kisiwa cha Lamu (kusini)
 8. Kimvita  – Mombasa na Kilifi
 9. Kijomvu, Kingare –  Mombasa
 10. Chifundi (Kishirazi) – Mombasa na Rasi ya Funzi
 11. Kivumba (Kivanga) – Mpakani mwa Kenya na Tanzania
 12. Kichwaka – Shimoni
 13. KiMtang’ata (Kimrima) – Tanga
 14. Kipemba – Kisiwa cha pemba
 15. Kiunguja (Kimji) – Zanziba mjini
 16. Kitumbatu – Kisiwa cha Tumbatu
 17. Kijambiani – Zanziba
 18. Kimakunduchi (Kikae) – Zanziba kusini
 19. Kimgao – Pwani ya kusini mwa Tanzania
 20. Kimwani – Kaskazini mwa Msumbiji
 21. Kingwana – Jimbo la Shaba la Zaire
 22. Kingazija – Kisiwa cha Komoro

Kuchangia kwa maoni hakujawezeshwa.