“Tenda Wema Nenda Zako”

“Tenda wema nenda zako.”

Kila anapoamka, mja huwa na tumaini la kutarazaki kwa fanaka na hatimaye kupata fedha atakazozitumia kugharamia mahitaji yake ya kila siku. Hujitolea kwa uwezo wake wote kung’ang’ana angalau apate lishe bora, mavazi na pahali pa kuishi. Hata hivyo, mengineyo huwa ni bahati yake.

Mwanadamu anapofanikiwa husahau mateso aliyoyapitia. Wengine huwapata marafiki wengine wanaowiana kwa hadhi na radhi. Hapo ndipo unaposikia kuwa kuna tajiri na maskini. Huyo maskini ndiye huyumba maishani akitafuta angalau ajikimu kimaisha. Tajiri naye kwa utajiri wake husahau kwamba kunao wanaokosa vya muhimu ili kufurahia maisha kama wao.

Kuna baadhi ya wale ambao huwakumbuka maskini na kuwasaidia kwa kidogo walicho nacho. Wengine hudai ni haki yao kuwa na mali bila kuwakumbuka wanaohangaika bila chochote.

Nilipoamka asubuhi hiyo nilitarajia kukutana na watoto wenye vipaji mbalimbali ila uwezo wao ni hafifu kwa kuwa wote ni mayatima. Nilijua kuwa si lazima tujitolee kuwaauni watu wa nasaba yetu au waliokuwa katika gatuzi langu.

Tarehe 30/7/2017 tuliandamana na masahabi wangu moja kwa moja ili kuwafaa mayatima ambao wanaaminika kuwa na uweza hafifu katika maisha yao. Ilikuwa wiki moja tu kabla ya Uchaguzi nchini Kenya na kila mtu alionekana kuwa na taswira moja tu – uchaguzi.

Mji wa Mũrang’a haukuwa tofauti. Huku ndiko walikokuwa wakimsubiri Naibu wa Raisi katika hafla ya kutawazwa kwa kasisi mmoja wa dhehebu la Kianglikana. Ilikuwa Jumapili na maduku makuu yalionekana kufungwa bila huruma yoyote kwa watu waliokuwa na ari ya kutenda wema.

Hatimaye tulibahatika kununua bidhaa ambazo zilionekana kuwa muhimu kwa yatima. Unapomfikiria mtoto kama huyo ni dhahiri kujua kuwa hana anayemwita mzazi. Wengine hukosa tumaini la maisha na kuona kana kwamba dunia imewageuka.

Eneo la Kangema, Mũrang’a lina mandhari njema na ya kupendeza. Milima na mabonde yanayowiana sambamba. Mabonde hupisha mito na milima hupisha barabara zinazosafirisha watu na shughuli zao.

Boma la watoto la Rehoboth linapatikana takriban kilomita 20 hivi mbali na mji huo wa Mũrang’a ukielekea Kangema. Hapo karibu mkabala na boma hilo la Rehoboth ndipo kuna Shule ya Upili ya Iyego. Hapa tulikutana wa watoto wengi na kuwapa tumaini la maisha kwa kuwatia moyo na kuwafaa kwa bidhaa mbalimbali. Watoto wanaoweza kutia bidii na kubadilisha maisha yao.

Mtoto kama huyo unapomtia moyo, hujibidiisha na kujiona kama mtoto mwingine yeyote aliye na uwezo. Huenda akawa kiongozi wa kesho. Unapombeza na kumvunja moyo atakosa tumaini la maisha na akose kujibidiisha. Si lazima uwe tajiri kuwa na ukarimu au kumsaidia yeyote anayehitaji msaada wako. Kidogo ulicho nacho kinaweza kubadilisha maisha ya mwengine hususan maskini, yatima, mjane nk.

 

Kuchangia kwa maoni hakujawezeshwa.