“Dadangu Ameshikwa!“

Si mara moja tumeona watu wamefariki kwa vichapo kutoka kwa askari wa baraza la jiji. Wengine wakiteswa na wanawake kubakwa kwa kukosa kutoa rushwa.

Nilikuwa mjini Eldoret katika pilkapilka za kutarazaki. Wakati mwingine uchovu huwa mwingi na cha muhimu sana ni amani. Hapana jingine ila kujikaza angaa kujipatia riziki ya kila siku. Ajizi ni nyumba ya njaa.

Niliabiri matatu zinazohudumu mjini kutoka eneo moja hadi jingine. Kando nami aliketi msichana aliyeonekana kuwa na umri wa miaka kumi na miwili hivi.

“Dadangu ameshikwa,” akalipuka kwa kilio cha kwikwi huku akiashiria nje.

Gari la askari wa utawala wa gatuzi lilipita huku wachuuzi wakiwa wamejaa sisisi. Huruma ikanizidia. Nikafikiria jinsi msichana huyo alivyomtegemea dadake kwa mahitaji yake ya kila siku. Kazi aliyoifanya ilikuwa imeshikwa mateka. Msaada wake ukawa umetoweka. Huenda ikawa hakuwa na mwengine wa kumsaidia au kumtoa dadake kutoka kwa mikono ya wahuni.

Wahuni hao huwatia nguvuni wachuuzi kwa madai kwamba wanavunja sheria za jiji. Hutegemea hongo ili wawaachilie huru. Wanaposhindwa au wanapokataa kutoa chai, huteswa, hubakwa na bidhaa zao huporwa.

Mungu amsaidie mja wake.

Kuchangia kwa maoni hakujawezeshwa.