Mshairi: Emmanuel Charo

Mshairi hufurahia anapotunga mashairi yatakayosomwa na watu wengi na bila shaka wamtie moyo wa kutunga zaidi. Kila mwendo ni hatua na hata safari ndefu huanzia kwa hatua. Hapa, tumebahatika kukutana na mshairi chipukizi, Emmanuel Charo, ambaye baadhi ya mashairi yake tumeyachapisha katika blogu zetu. Haya hapa mahojiano yetu.

Tuelezee kwa kifupi Emmanuel Charo ni nani.
Emmanuel Charo Katana almaarufu “Malenga Daktari ” ni mzawa wa tarehe 21/8/1997 katika kitongoji cha Maryango kaunti ya Kilifi lakini kwa sasa naishi Mombasa.

Ulisomea wapi na miaka gani?
Nilisomea elimu yangu ya msingi katika shule za Maryango, Changamwe na Bethsaida kati ya miaka ya 2003-2012. Nilipata elimu yangu ya upili katika shule ya kitaifa ya Kenyatta, Taita, (2013-2016) kisha nikapata mwaliko wa kusomea shahada ya uafisa wa kliniki (BSc. Clinical Medicine) katika chuo kikuu cha sayansi na teknolojia cha Meru (MUST) ambako ninatarajia kufuzu mwaka wa 2021.

Ulianza kutunga mashairi lini na ni nini ilichangia?
Nilianza kutunga mashairi nilipokuwa kidato cha nne (2016).Hii ilitokana na hamu niliyokuwa nayo kwa lugha ya Kiswahili na ushairi. Nilikuwa nawapenda sana watangazaji kama vile:
1. Ali Hassan Kauleni – Radio Maisha “Nuru ya lugha”
2. Mkalla wa Mwambodze-Bahari fm “Kutubuti”
3. Mrinzi Nyundo Mrinzi – Radio Kaya “Malenga wa Kaya”

Ni mshairi gani ambaye unaweza kuvulia kofia?
Mshairi ambaye alinivutia sana ni Mwinyi Bokoko hasa kwa mashairi yake ya kispoti na sauti yake ya dhahabu bila kumsahau Nuhu Zuberi Bakari.

Unaweza kulikumbuka shairi lako la kwanza?
Shairi langu la kwanza kulitunga linaitwa “Kimahaba Sioni” na kutokea hapo nimetunga mashairi kama manane.

Wewe hutunga mashairi ya aina gani?
Ninajihusisha na kutunga mashairi aina ya tarbia na hasa bahari tofautitofauti hasa ukaraguni. Mimi hupendelea kuandika mada za mapenzi, matukio ya hivi sasa, na sifo.

Lengo lako ya siku za usoni ni gani?
Lengo langu kuu ni kuelimisha jamii na kuibadilisha msimamo wake kuhusu ushairi na hali kadhalika kuchapisha diwani yangu ya mashairi. Vilevile kupata fursa kukariri au kuimba mashairi kwenye matamasha, vyombo vya habari. Hali kadhalika ningependa kuhusika katika kuwaunganisha washairi katika nchi yetu.

Washauri washairi chipukizi.
Ushauri wangu kwa washairi chipukizi kama mimi ni kuwa wazidi kutunga mashairi yao na wasikate tamaa katika harakati zao za kusaka soko ya sanaa yao.

Mashairi ya Emmanuel Charo

Unaweza kuwasiliana na Emmanuel Charo kwa njia zifuatazo:

  1. Rununu: +254724250972
  2. Baruameme: drcharoemmanuel@gmail.com
  3. Facebook: Daktari Charo

Kuchangia kwa maoni hakujawezeshwa.