Wosia kwa Mwanao

Mwambie mwanao afanye kazi kwa malengo na kujituma kiwango cha salio lake la banki siku moja lifafane na namba zake za simu. Mwambie awe na nidhamu ya pesa na ajenge utamaduni wa kutunza pesa na kuweka akiba.

Mwambie aige kutafuta pesa na asiige matumizi. Mwambie aipende pesa kwa vitendo na sio kwa hisia. Kila mtu hapa duniani ana hisia kwamba kuna siku atafanikiwa katika maisha yake. Ila wanaopata hiyo bahati ni wale wanaoishi kwa malengo, kujituma na kuhangaika. Hakuna siku mbingu itafunguka na mikate ishuke kutoka angani. Hakuna dhambi mbaya kama uoga

Mwambie hata siku moja asiogope kudai haki yake. Msisitizie kwamba, kama akifanya kazi ambayo inashaliza pesa na mwishowe asipate kitu chochote ajue dhahiri kwamba kuna mtu amepata. Na ikiwa ameajiriwa, mwambie atumie kipato chake kwa malengo na kwa makini sana.

Asije akafanya kazi ili apate pesa. Alinunue gari ili alitumie kuendea kazini. Atachelewa sana. Mwambie ajifunze kununua vitu vinavyozalisha pesa nje ya ajira, ili siku moja aweze kujitegemea kiuchumi.

Mwambie mwanao Mwenyezi Mungu amempa akili ili aitumie kutatua matatizo yake, na akiitumia vibaya atatengeneza matatizo zaidi kuliko kutatua.

Utakapokuwa unaongea naye naomba umwambie asiwe na tamaa hasa ile ya kutamani watu wengine. Kwa sababu ni ngumu sana kujua uhalisia wake.

Sisi binadamu ni kama mwezi. Tuna upande wenye giza na upande wenye mwanga. Siku zote watu huona upande wenye mwanga tu. Upande wenye giza daima hubaki kuwa siri.

Nakuomba umfundishe mwanao namna ya kufikiri na si nini cha kufikiri. Ili kesho na kesho kutwa asije kuwa na fikra ndogo kama kenge anayekimbia manyunyu ya mvua na kuingia mtoni ili asilowe. Na zaidi ya hayo, usiache kumfundisha kuhusu akili za watu na matendo yao katika mwitikio dhidi ya ujuaji wa mambo.

Na hapo umwambie hivi, mjinga hajui kitu na hajui kama hajui. Mjaja anajua kitu na anajua kama hajui. Mshenzi anajua halafu anajifanya hajui. Na mpumbavu yeye hajui halafu anajifanya anajua.

Mwambie siku zote wanavyolalamika jinsi mpira unavyodunda, mara nyingi ndio hao hao walioudundisha.

Mwambie kuishi na watu ni kazi kubwa inayohitaji umakini sana. Na ili afanikiwe katika hilo, mkumbushe kwamba Mwenyezi Mungu alimuumba mwanadamu na masikio mawili na mdomo mmoja. Maana yake ni kwamba siku zote mwambie anasikiliza zaidi kuliko kuongea. Na kamwe asijali maneno mabaya ya watu dhidi yake kwani mtu hawezi kuzuia watu wasiseme. Ila unaweza kuzuia mdomo wako usiseme.

Mwambie mwanao kila wakati atakaposimama katika kundi la watu wengi, ni vigumu sana kukubalika na watu wote. Na vigumu pia kuchukiwa na watu wote. Kwa mfano, atakaposimama kati ya kundi la watu mia moja, basi walau watu kumi na watano watampenda, kabla hajafanya chochote. Na watu kumi na watano watamchukia kabla hajafanya chochote. Watu sabini waliobaki watampenda au kumchukia kutokana na kile atakachokifanya. Mwambie kwamba hawezi kupendwa na watu wote au kuchukiwa na watu wote.

Mtie moyo mwanao kwa kumweleza kuwa matatizo ni sehemu ya maisha. Kwani hata dhahabu hupitishwa kwenye tanuu la moto kabla haijang’ara. Hivyo akiona matatizo yanamwandama basi ajue neema inakaribia. Hata Waswahili walipata kusema, ukiona kiza kimezidi jua kumekaribia kupambazuka.

Maisha yana furaha na matatizo. Na maisha yana raha kwa sababu ya matatizo. Mwambie mwanao, uchungu wenye chungu ndio utamu wenyewe eti.

Mwambie kuna namna kuu mbili za kukabiliana na Changamoto. Ya kwanza ni kuitatua au kuibadilisha changamoto na ya pili ni kubadilika yeye ili aendane na Changamoto. Na hapo umkumbushe kwamba mara nyingi mtu unaposhindwa kulitamka neno, huwa inakulazimu kufikiria sentensi mpya, ili tu kuliepuka hilo neno.

Haya yote ninayokuambia naomba umfundishe wewe. Haina haja ya kungojea hadi ulimwengu umfundishe. Watu siku hizi si wema tena na hawana upendo kama zamani. Mfano, unaweza kufanya harambee ya kuchangia ujenzi wa bwawa la kuogelea na mtu akakuletea ndoo moja ya maji kama mchango wake. Mwambie asitegemee watu wengine kufanya mambo yake ya msingi. Kwa hivyo basi jambo lolote ambalo anaweza kulifanya mwenyewe asisumbuke ili afanyiwe na watu. Na usisite kumwelimisha ya kwamba, chanzo cha furaha yake siku zote ni yeye mwenyewe. Na akiwa na mazowea ya kutegemea watu wengine, ndio wawe chanzo cha furaha yake, inaweza ikawa kinyume chake.

Utakapokuwa ukimwambia maneno haya, usisahau kumkumusha kujifunza na kujaribu mambo mengi katika maisha yake. Mwambie ni heri kufanya kitu na kujutia baadaye, kuliko kuja kujuta kwa kutokifanya.

Mwambie elimu bora haipatikani shuleni tu. Ajifunze na elimu ya mtaani pia. Kuwa na marafiki ni kitu kizuri ila kuwa na marafiki wabaya ni bora kuwa peke yake. Mwambie marafiki atakaochagua ndiyo itakuwa taswira yake. Na atakuwa kama wao. Na kamwe asijadili matatizo yake na watu walioshindwa kutatua matatizo yao.

Yapo mambo mengi sana ambayo nilitamani umwambie. Lakini muda si rafiki sana. Kwa leo naomba umwambie hayo tu. Ikiwa atakuuliza swali lolote kuhusu haya niliyokwambia halafu likakushinda, basi nipigie simu tuongee naye.

Na iwapo atakuuliza maswala ya mapenzi, mahusiano au ndoa, mwambie unahitaji muda usiopungua wiki moja ili kujadili hiyo mada kwa ufupi. Ila kwa leo, akikuuliza mapenzi ni nini, mujibu kwa ufupi sana kwamba mapenzi ni hisia zinazoumiza, ambazo hazichoshi. Na akikuuliza ni namna gani ya kupata mchumba anayefaa, kwa ufupi sana mwambie mchumba mzuri hachukuliwi ila anachaguliwa.

Shukran.

Kuchangia kwa maoni hakujawezeshwa.