Ninaweza Kutunga!

Si kwamba ulizaliwa ukiwa bingwa. Ufanisi huja kwa hatua za jitihada. Unaposikiliza watu na kuyaamini, huenda ukafa moyo au ukawa na nguvu na ujasiri wa kuendelea. Leo ningependa kuwatia moyo washairi chipukizi walio na ari ya kutunga ushairi bora.

Nilianza kutunga mashairi nikiwa darasa la tano katika shule ya msingi ya Gatei, jimbo la Kiambu. Hii ilikuwa ni baada ya kusoma mashairi yaliyokuwa kwenye msururu wa vitabu “Kiswahili kwa Darasa.” Katika nyakati hizo, nilitunga tu mshororo ambayo mizani hazikuwiana na vina havikufanana. Ilikuwa mshororo jina tu. Sikujua siku moja kwamba nitaweza kutunga shairi.

Mashairi yaliyochapishwa kwenye gazeti la “Taifa Leo” yalinichochea ajabu. Ikawa mazoea ya kulinunua gazeti lenyewe lililopatika kwa nadra sana vitongojini. Ndizo nyakati nilikuwa nikitembea kilomita kama kumi hivi angaa kujitafutia nakala yangu.

“Ninaweza kutunga!” hisia zangu zikanifokea licha ya kwamba nilijiona kwamba siwezi. Kuanzia siku hiyo, nilituma mashairi kwa wingi kwa Gazeti la hilo ila hayakuchapishwa. Sikujua sababu iliyochangia kutochapishwa kwa mashairi hayo ila niliapa kujikaza bila kufa moyo. Nilijua kwamba hata kama hayakufikia kiwango cha kuitwa mashairi, siku moja ingekucha tu. Sababu inayotufanya kutofaulu, ni kukosa subira na kufa moyo kwa urahisi.

Hatimaye mashairi yangu yalichapishwa na gazeti hilo jambo ambalo lilinitia moyo zaidi nikaweza kutunga kwa wingi. Sisemi kuwa mashairi yangu ni bora kiasi cha haja, ila najua ni bora kuliko yalivyokuwa miaka ishirini iliyopita. Ninapoandika makala haya, nimetunga mashairi yasiyopungua mia tano. Baadhi ya mashairi hayo yamechapishwa na magazeti mbalimbali, yamepeperushwa na redio kadhaa nchini Kenya na nje. Mengine yametumika katika shule kwa wanafunzi wa Kiswahili. Ni tumaini langu kuwa mashairi yangu yatazidi kuwafaa wanafunzi na wapenzi wote kwa jumla wa ushairi.

Katika safari hii, singeweza pasi na msaada wa magwiji mbalimbali akiwemo marehemu Omar Babu Marjan aliyenifaa sana kunifafanulia sheria za utunzi. Alinisaidia na kunipa moyo, jambo ambalo hadi leo lingali linanishawizi kuendelea kutunga mashairi.

Unapotenda jambo lolote, usitende kwa lengo la kunufaika kifedha. Jaribu kutoa mchango wako kwa jamii, jambo ambalo litasaidia mwenzako. Uliko sasa hivi, si kwa uwezo wako mwenye. Ni kwa nguvu za Mwenyezi Mungu. Pia kunao washika dau na watu mbalimbali waliochangia ili uweze kutimiza azma yako.

Zifuatazo ni baadhi ya mbinu zitakazokufaa katika utunzi wa mashairi
1. Kusoma mashairi ya wengine na kujaribu kuiga ushairi ulio bora.
2. Kufanya utafiti kwa makini kuhusu ushairi; historia, maana, istilahi, uhuru wa mshairi, nk.
3. Kufanya mazoezi ya kutunga mara kwa mara.
4. Kujihusisha katika makongamano yanayozungumzia mada za ushairi.
5. Kusikiliza vipindi vya redio vinavyoelezea mengi kuhusu utunzi wa mashairi.
6. Kusikiliza wabuji wanaoghani mashairi.

Hizo tu ni baadhi ya njia zitakazokusaidia kuinua kiwango chako cha utunzi wa mashairi.

Katika tovuti hii utasoma mengi kuhusu ushairi. Unaweza pia kupitia mafunzo yetu ya Utunzi wa Mashairi usome hatua kwa hatua jinsi mashairi hutunga.

Kuchangia kwa maoni hakujawezeshwa.