Mshairi: Vincent Okwetso

Vincent Okwetso alizaliwa Butula, Kaunti ya Busia. Ni mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia cha Masinde Muliro, katika kaunti ya Kakamega anakosomea ualimu.

Vincent alianza kutunga mashairi mwaka 2017 mwezi wa kumi tarehe 26, ambapo ilikuwa siku ya marudio ya kupiga kura zilizokuwa zimefanyika mwezi wa nane tarehe nane mwaka 2017. anakumbuka vyema akiwa Nairobi, kura za kwanza zilipofanyika , yaliyomfanyikia anasema ni huzuni sana kuyaeleza. Katika marudio hayo ya kupiga kura ya pili ya urais, alijipata akiimba na kuimba huko, mtiririko fulani ulijitokeza; akajaribu kuandika chini. Anadai hapo ndipo alijua kweli anaweza kutunga mashairi.

“Nakumbuka vyema sana nikiwa darasa la tano; nilikuwa napenda sana kuimba beti za mashairi mbalimbali. Kuna shairi katika kitabu cha kiswahili mufti cha darasa la tano lenye mada ‘MOYO WANAMBIA’. Shairi hilo ndilo lilinipatia ari ya kuanza kuyakariri mashairi mengine na hadi mwaka wa 2017, mwezi wa 10 tarehe 26, nikalitunga shairi langu la kwanza.”

Washairi ambao anaowavulia kofia ni Bw. Kitula King’ei, katika Diwani yake ya Miale ya Uzalendo, Shabani Robert bila kumsahau Profesa Ken Walibora.

Shairi lake la kwanza lilikuwa kuhusu amani. Aliomba sana kusitokee rabsha katika marudio hayo ya kura ya urais. Hili hapa Shairi lake la kwanza kulitunga;

Amani Kenya

Mungu baba twakuomba, tujalie amani,
Dua zetu sigonge mwamba, twa’mba nchi yenye amani
Tupe baraka Muumba nchi yetu yenye amani
Twaomba umoja nchini, nasi kwako ‘we imani.

Maombi yetu twaleta, twaombaa upokee
Amani bila utata, Muumba utujalie
‘Ongozi bila matata, Rabana tupokezee
Twaomba umoja nchini, nasi kwako ‘we imani.

Tamati nakaribia, zangu salaa pokea
Mwisho hatujafikia,pokea zetu duaa
Tujalie barakaa, kwetu ‘we kutujengaa
Twaomba umoja nchini, nasi kwako ‘we imani.

Ukingoni ‘mefikaa, tumaini zetu kwako
Twakesha kwenye salaa, tukiomba nema zako
Asante sana Mumbaa, twaona matendo yako
Twaomba umoja nchini, nasi kwako ‘we imani.

© Vincent Okwetso

Bahari za mashairi ambayo anajihusisha nayo kwa wingi ni kama bahari ya utenzi, mathnawi, mkufu na ukaraguni. Kwa sasa, ameweza kuyatunga mashairi kumi la kwanza likiwa hilo la Amani Kenya. Anasema mada anayotungia mashairi kwa wingi ni Elimu. Ingawa hilo la Amani Kenya si la Elimu, linaelimisha viongozi dhidi ya uongozi mbaya. Angependa kuwaelimisha waja juu ya mambo mengi yanayotendeka mwiongoni mwetu sisi wanadamu; kwa mfano, katika Shairi lake la Ulimi Kiungo Dhaifu, anaeleza vyema jinsi ndimi zetu zinapaswa kutumika.

Lengo lake kuhusu upeo wa usanii ni kuwa angependa kukuza kipawa chake cha ushairi aweze kuandika Diwani yake ili isomwe na wengi wanaopenda mashairi. Miaka kumi ijayo, ambapo itakuwa mwaka wa 2028 angependa kuwa mhakiki wa mashairi na kuwa na Diwani yake binafsi au kwa ushirikiano na waandishi wengine wa mashairi.

“Ningependa kuwahimiza wenzangu ambao wanaanza kutunga mashairi, waweze kutia bidii katika utunzi wao; na pia wapende kazi yao ya utunzi ili siku moja utunzi huo uweze kuwa kibarua cha kuwachumia unga.”

Soma Mashairi yake hapa

Kuchangia kwa maoni hakujawezeshwa.