Kuhusu Mwandishi

Kimani wa Mbogo, anayejulikana kwa lakabu Mwanagenzi Mtafiti, alizaliwa Mbichi, Gatundu. Alisomea Shule ya Upili ya Mbichi kabla ya kujiunga na vyuo mbalimbali kwa masomo ya uhasibu.

Huko shuleni Mbichi, ndiko alianza uandishi na utunzi wa mashairi. Utunzi wake ulikumbwa na matatizo si haba. Kimani alikua kwenye mazingira ya watu wasiouthamini ufasaha wa Kiswahili na utunzi wa mashairi. Maarifa na ufundi alioupata wa kutunga mashairi, ni kutokana na vitabu na magazeti aliyoyasoma na kusikiliza vipindi redioni.

Kimani alifunza somo la Kiswahili katika shule mbalimbali kama Vineyard Joy Academy (2005) na Gatei Joyland Academy (2006-2008) alikokuwa naibu wa mwalimu mkuu. Hamu yake ya kuwa mwalimu wa Kiswahili hatimaye ilikuwa imetimia. Wakati huo, Kimani aliweza kufanya utafiti kwa masuala tofauti ya ushairi na lugha ya Kiswahili. Aliweza kutunga mashairi aliyotumia kwa wanafunzi wake kuhakiki.

Aliomba dua tungo zake zichapiswe kutwa moja kwenye majarida, magazeti, vitabu na redioni, jambo ambalo limetimia. Licha ya kujaribu jambo hilo kwa muda mrefu tangu alipokuwa mwanafunzi shuleni Mbichi, ndoto yake Kimani sasa imetimia. Kwa sasa amechangia kwa mashairi yake kwenye idhaa mbalimbali nchini Kenya (QFM, KBC, Radio Maisha na Sauti ya Amerika). Baadhi ya mashairi yake yamefanyiwa uchambuzi na kuzua mijadala redioni. Mengine yameghaniwa na magwiji watajika Abdallah Mwasimba (KBC). Majarida na magazeti mbalimbali kama Taifa Leo pia yamechapisha mashairi yake kwa muda mrefu tangu mwaka wa 2005.

Kwa sasa, Kimani ni mfanyikazi katika Shirika Lisilo la Kiserikali linalojihusisha na miradi dhidi ya umaskini katika jamii.